Katika kuendeleza kasi ya uwajibikaji na nidhamu ya kazi , serikali ya Tanzania imezindua mfumo mpya wa kielektroniki wa usajili wa wafanyakazi wa serikali nchini humo
Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa amezindua mfumo huo wa kielektoniki utakaotumika katika kusajili wafanyakazi wa Serikali pindi waingiapo na watokapo maofisini lengo likiwa ni kuboresha na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Waziri Profesa Mbarawa Amesema kuwa kuwepo kwa mfumo huo katika ofisi mbalimbali za serikali kutasaidia wafanyakazi kuingia na kutoka maofisini kwa wakati hivyo kupunguza tatizo la uchelewaji na utoro.
Tatizo linaelezwa limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya nchi na kufanya uchumi wa nchi kushindwa kuongezeka.
Mfumo huo wa kielektroniki wa kusajili wafanya kazi wa serikali utaanzia ndani ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Idara zote za Wizara hiyo na baadaye kutumika katika ofisi na taasisi zote za Serikali
Tokea kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano chini ya rais Dakta John pombe magufuli hatua kadhaa zimefanyika kuboresha uwajibikaji na utendaji kazi katika idara mbalimbali za serikali huku viongozi kadhaa waliobainika kuzembea wakichukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria.
Tayari wafanyakazi wote wa serikali wameamriwa kuweka BEJI yenye majina yao katika mavazi ili watanzania waweze kutambua nani anawahudumia kwa wakati husika.
Your browser doesn’t support HTML5