Tanzania yaruhusu ndege za Kenya kutua

Ndege ya shirika la Kenya Airways safarini

Hatua hii imefuatia uamuzi wa Kenya Jumanne kuruhusu Watanzania kuingia Kenya bila kukaa karantini ya siku 14

Serikali ya Tanzania imeondoa marufuku iliyokuwa imeyawekea mashirika ya ndege ya Kenya kutoingia nchini humo, na sasa ndege za Kenya, ikiwemo shirika kuu la Kenya Airways (KQ), zinaweza kufanya safiri za kwenda na kurudi Tanzania.

Mamlaka ya safari za anga Tanzania TCAA, imesema katika taarifa fupi Jumatano kuwa imeondoa marufuku hiyo, siku moja baada Kenya kuijumuisha Tanzania katika orodha mpya ya nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia Kenya bila kukaa karantini ya siku 14.

Mgogoro wa safari za ndege ulianza August 1 Kenya ilipotoa orodha ya kwanza ya nchi zilizoruhusiwa kuingia Kenya bila karantini na kuiwacha Tanzania nje ya orodha hiyo. Mara moja Tanzania ilijibu kwa kuondoa ruhusa kwa shirika la KQ kutua katika viwanja vya Tanzania. Marufuku hiyo ilidumu kwa miezi miwili.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na mkurugenzi mkuu wa TCAA Hamza Johari imesema kwamba Tanzania “imechukua hatua ya kuondoa marufuku hiyo baada ya Kenya kuondoa marufuku ya kutaka wasafiri kutoka Tanzania kuwekwa karantini ya siku 14.”

Taarifa hiyo inaendelea kusema kwamba “kwa ajili ya kujibu hatua hiyo kwa kiwango sawa, Tanzania itaondoa marufuku iliyowekewa ndege zote kutoka Kenya ambapo ni Pamoja na Kenya airways, Fly 540 limited, Safarilink Aviation na AirKenya Express Limited, na kwamba ndege hizo zinaweza kurejea safari zake mara moja.

Nchi hizo zimekuwa na mbinu tofauti ya namna ya kupambana na janga la virusi vya Corona, Tanzania ikisisitiza kwamba hakuna virusi vya Corona kabisa nchini humo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC