Polisi nchini Tanzania wamethibitisha Jumanne kuwa wanamshikilia mwandishi wa habari Erick Kabendera ambaye Jumatatu iliripotiwa kuwa amechukuliwa na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es salaam Jumanne kuwa Kabendera anashikiliwa kuhojiwa kuhusu uraia wake. Mambosasa alisema polisi ililazimika kumkamata Kabendera baada ya kushindwa kuripoti kituo cha polisi kama alivyotakiwa.
Kabendera, mwandishi wa habari za uchunguzi katika magazeti ya ndani na nje ya nchi, alikamatwa nyumbani kwake Jumatatu katika mazingira yaliyozusha wasiwasi kwamba waliomchukua sio polisi baada ya polisi kusema hawana habari yoyote kuhusu kukamatwa kwa mwandishi huyo.
Baada ya habari kuanza kuripotiwa katika vyombo vya ndani na nje ya nchi pamoja na mitandao ya kijamii polisi katika wilaya ya Kinondoni, Dar es salaam, walithibitisha Jumatatu usiku kuwa mwandishi huyo amekamatwa na yuko mikononi mwa polisi.
Ndugu wa Kabendera wanasema mwandishi huyo alizaliwa Bukoba, mkoa wa Kagera, mwaka 1980. Alikwenda chuo kikuu cha Dar es salaam, na ameishi maisha yake yote nchini Tanzania.