Kenya yaruhusu Watanzania kuingia nchini humo bila karantini

Abiria waliovalia barakoa wakiwasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi, August 1, 2020.

Hatua hiyo huenda ikafungua mazungumzo kuhusu safari za ndege baina ya Kenya na Tanzania

Hatimaye serikali ya Kenya imeiorodhesha Tanzania kati ya nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia nchini humo bila kulazimishwa kuwekwa karantini ya siku 14 kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Nchi zote za Afrika Mashariki sasa zimejumuishwa kwenye orodha mpya ya nchi 147 iliyotolewa Jumanne.

Hatua hiyo mpya ya Kenya huenda ikafungua njia ya kupata suluhu katika mvutano wa Tanzania na Kenya uliosababisha Tanzania kufuta kibali cha ndege za Kenya kutua nchini Tanzania. Shirika la ndege la Kenya KQ pamoja na mashirika mengine yamezuiliwa kutua katika viwanja vya Tanzania kwa miezi miwili sasa.

Orodha hiyo ya Kenya ni ya pili tangu serikali ya nchi hiyo ilipoanza kufungua shughuli zake za kawaida ikiwemo usafiri wa ndege kwa safari za kimataifa.

Kando na Tanzania, nchi nyingine ambazo zimeongezwa kwenye orodha mpya ni Burundi, Ghana, Nigeria na Sierra Leone

Kenya ilirejesha safari za ndege za kimataifa Agosti 1 kwa kuruhusu wasafiri kutoka nchi 11 pekee kuingia nchini humo bila kuwekwa karantini ya lazima kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Orodha hiyo iliongezwa hadi 130 mnamo Agosti 19, lakini Tanzania haikuwa katika orodha hiyo, jambo ambalo lilisababisha hisia kali kutoka kwa serikali ya Tanzania ambayo ilijibu kwa kufuta leseni ya Kenya Airways kutua katika ardhi ya Tanzania.

Chanzo cha mgogoro kati ya Kenya na Tanzania

Mgogoro kati ya Kenya na Tanzania ulianza pale mlipuko wa virusi vya Corona ulipotangazwa kuwa janga la kitaifa na nchi kadhaa kuanza kuweka mikakati ya kuepusha raia wake dhidi ya maambukizi.

Kenya, pamoja na nchi zingine za Afrika mashariki, zilianza kutekeleza makubaliano ya kupima madereva wote wa magari ya kubeba mizigo mipakani, lakini Tanzania haikuwa sehemu ya makubaliano hayo na hivyo kuzua mgogoro wa mpakani kati ya Kenya na Tanzania.

Wageni ambao vibali vyao vimepitwa na wakati watakiwa kuondoka

Wakati huo huo Idara ya Uhamiaji ya Kenya imeondoa msamaha uliowaruhusu raia kutoka nchi zingine kuishi nchini humo bila kibali, baada ya muda wao wa kuwa nchini kukamilika, kutokana na janga la virusi vya Corona.

Taarifa ya mkuu wa idhara ya uhamiaji Alexender Muteshi, inataka raia wote wasiokuwa na vibali kuondoka nchini humo mara moja.

Muteshi amesema kwamba hatua hiyo inafuatia Kenya kufungua anga yake kwa ufasiri wa kimataifa.

“kufuatia hatua ya kuondolewa kwa masharti ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona na kuanza tena kwa safari za ndege kimataifa, idara ya uhamiaji imeondoa msamaha uliokuwa umtolewa kwa raia wa kigeni ambao vibali vyao vya kuwa nchini vimepitwa na muda” imesema taarifa hiyo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC