Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Iran IRNA, limeripoti kwamba mapigano yametokea kwenye mpaka wa Sistan, jimbo la Baluchistan na jimbo la Nimroz nchini Afghanistan.
Ripoti ya shirika hilo imesema kwamba vifo kadhaa vimetokea, na pia uharibifu mkubwa.
Vyombo vya habari vya Afghanistan, vinavyodhibitiwa na Taliban, havijaripoti kuhusu tukio hilo.
Kundi la wanaharakati la HalVash, ambalo huripoti kuhusu maswala yanayohusu wabaluch katika jimbo la Sistan na Baluchestan, lenye Wasunni wengi, limenukuu wakaazi wa sehemu hiyo wakisema kwamba mapigano yameanza Jumamosi asubuhi.
Mapigano hayo yametokea baada ya rais wa Iran Ebrahim Raisi kuionya Taliban mapema mwezi huu, dhidi ya kuingilia haki ya Iran kutumia maji ya m to Helmand.
Iran imekabiliwa na ukame kwa muda wa miaka 30. Idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Iran imesema kwamba karibu asilimia 97 ya nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya ukame.