Takriban watu 200 wakamatwa kwenye maandamano dhidi ya Israel, New York

  • VOA News

Picha ya baadhi ya waandamanaji waliozuiliwa Jumatatu New York, Oct. 14, 2024

Takriban waandamanaji 200 waliokuwa wakipinga vita vya Israel huko Gaza Jumatatu walikamatwa wakiwa wameketi nje ya jengo la biashara kuu za hisa mjini New York.

Waandamanaji hao, wakiwa nje ya jengo hilo maarufu lililopo kwenye kitongoji cha Manhattan, walisikika wakisema kuwa “Let Gaza Live” Up up with liberation, down down with occupation,” ambazo ni kauli za kutetea uhuru wa wakazi wa Gaza na kupinga mashambulizi yanayoendelea kutekelezwa na Israeli.

Beth Miller ambaye ni mwanaharakati wa kisiasa kwenye kundi la Jewish Voice for Peace, ambalo liliitisha maandamano hayo alisema kuwa, “Sababu yetu kukusanyika hapa ni kuomba Marekani isite kutuma mabomu kwa Israel, na ikome kufaidi kutokana na mauaji ya halaiki wapalestina yanayotekelezwa na Israel.”

Wakati huo huo kundi ndogo la waandamanaji wakiwa na vibendera vya Israel walionekana karibu na kundi hilo lililokuwa likipinga Israel. Kwenye ripoti tofauti Shirika la Msalaba mwekundu la Lebanon lilisema Jumatatu kwamba shambulizi la anga la Israel liligonga jengo la makazi kaskazini mwa Lebanon na kuuwa takriban watu 21.