Taasisi ya moyo Tanzania yashirikiana na madaktari bingwa

Dkt Bashir Nyangasa, bingwa wa upasuaji akimpima mgonjwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete

Moja ya mafanikio ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ni kufanikisha kuwepo ushirikiano na hospitali na taasisi mbalimbali za moyo kutoka nje ya Tanzania kwa ajili ya kubadilishana ujuzi ikwemo Uingereza, Marekani, Israel , India , Saudi Arabia na Australia

Mmoja wa wataalam wa moyo kutoka Mumbai India ambaye yupo hivi sasa kwenye Taasisi hiyo kwa ajili ya kambi maalum ya upasuaji wa moyo Dkt Ali Asgar amesema kwa sasa wataalam wa taasisi hiyo wanahitaji kupata tu mafunzo ya kina ili kuwezesha kufanya vizuri zaidi.

Naye Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, anasema upasuaji huo nchini umeweza kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi ikiwemo nchini India.

Amekiri bado taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikwemo upungufu wa vifaa na ukosefu wa umeme wa uhakika.

Kwa upande wake mtaalam wa dawa za usingizi, Dkt Angela Muhozi anasema kuwa kwa mara ya kwanza toka ianzishwe taasisi hiyo ya moyo ya Jakaya Kikwete imeweza kufanya operesheni kubwa ya kurekebisha mshipa mkubwa wa moyo.

Ameeleza operesheni hiyo ambayo siku za nyuma ilikuwa ikifanyika nje ya nchi, sasa inafanyika katika taasisi hiyo.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa baadhi ya wagonjwa waliopata matibabu kwenye taasisi hiyo ya moyo ya Jakaya Kikwete wametoa ushuhuda wa huduma walizopokea na kuwataka watanzania kuwa na imani na matibabu ya taasisi hiyo ya moyo.

Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa sasa ina vyumba vinne vya upasuaji vinavyowezesha kufanya operesheni za kuzibua mishipa, kuweka vyuma kwenye moyo, pacemakers, kuziba matundu bila kupasua kifua na magonjwa mengine ya moyo

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilianza rasmi upasuaji wa moyo mnamo mwaka 2008 katika taasisi ya mifupa na mishipa ya fahamu MOI, AMBAPO walikuwa kwa mwaka wanapasua wagonjwa 50.

Hata hivyo, Taasisi hiyo ya Jakaya Kikwete mwaka 2015 ilihamia rasmi kwenye majengo yake ambapo ufanisi uliongezeka zaidi na kuwezesha kupasua zaidi ya wagonjwa 300 kwa mwaka.