Ukame mbaya sana huko Pembe ya Afrika kuwahi kutokea katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 unaonekana kuwa utakuwepo kwa muda mrefu ujao, baadaya Taasisi ya Hali ya Hewa Duniani (WMO) kusema Ijumaa kwamba utabiri kwa miezi ya Oktoba mpaka Desemba unaonyesha kuwa kuna nafasi kubwa ya kuwepo na hali ya ukavu zaidi kuliko hali ya wastani ilivyo.
Mtizamo wa karibuni unathibitisha khofu iliyotolewa na mashirika ya misaada ambayo yamekuwa yakionya kwa miezi kadhaa kuhusu matokeo mabaya ya ukame kwa Ethiopia, Somalia na sehemu za Kenya, ikiwa ni pamoja na hatari ya njaa kwa Somalia.
“Kwa bahati mbaya, mifano yetu inaonyesha kuwa kiwango kikubwa cha imani kwamba tunaingia katika mwaka wa tano mfululizo wa msimu wa tano wa mvua zisizo za kawaida huko Pembe ya Afrika,” alisema Guleid Artan, Mkurugenzi wa Masuala ya Hali ya Hewa katika IGAD (ICPAC), kituo cha hali ya hewa cha WMO kwa Afrika Mashariki.
“Nchini Ethiopia, Kenya na Somalia, tuko kwenye hatari ya kupata janga lisilotarajiwa la kibinadamu,” aliongezea.
Ukame umeingiliana na kupanda kwa bei za vyakula na mafuta ulimwenguni, na kusukumwa pia na vita nchini Ukraine, ambapo mataifa mengi ya Afrika yamepigwa vibaya sana. Benki ya Dunia ilisema mwezi Juni kwamba inakadiriwa kuwa watu milioni 66.4 huko Pembe ya Afrika walitarajiwa kupata matatizo ya chakula au mgogoro mkubwa sana wa chakula, dharura, au njaa ifikapo mwezi Julai. Makadirio mapya kulingana na utabiri wa karibuni hayakuweza kupatikana mara moja.