Anakuwa waziri mkuu wa tatu katika muda wa mwaka mmoja, baada ya kujiuzulu kwa Liz Truss.
Sunak, anaingia madarakani wakati Uingereza inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi huku mamilioni ya watu nchini Uingereza wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu na nishati.
Sunak mwenye umri wa miaka 42, amekutana na mfalme Charles wa III, aliyeidhinisha uteuzi wake, muda mfupi baada ya kupokea rasmi ombi la Liz Truss kujiuzulu.
Anakuwa waziri mkuu wa Uingereza mwenye umri wa chini zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka 200.
Anatarajiwa kuanza kuunda baraza lake la mawaziri litakalofanya kazi kuhakikisha kwamba Uingereza inatoka kwenye mgogoro wa uchumi. Ana kazi pia ya kujaribu kukiunganisha chama cha Conservative ambacho kimegawanyika baada ya kujiuzulu kwa Truss na kilichoingia katika mgogoro mkubwa na kupelekea kujiuzulu kwa Boris Johnson.
Akizungumza katika makao ya waziri mkuu mjini London, Sunak amesema kwamba Truss alifanya makosa katika baadhi ya maamuzi yake lakini akaahidi “kurejesha udhibiti wa uchumi na Imani ya watu wa Uingereza”.
Amesema kwamba “atakabiliana na mgogoro wa kiuchumi” kwa kuongoza serikali kwa “uadilifu, weledi na uwajibikaji.”