Sunak anagombea nafasi hiyo pamoja na waziri mkuu wa zamani Boris Johnson na aliyekuwa waziri Penny Mordaunt.
Kuna hali ya sintofahamu, baada ya vyombo vya habari vya Uingereza kuripoti kwamba Sunak amefanya mazungumzo na Boris Johnson na kwamba huenda wawili hao wakatangaza ushirikiano kwa lengo la kukiunganisha chama cha Conservative ambacho kimegawanyika baada ya kuanguka kwa utawala wa muda mfupi wa Liz Truss.
Chama cha Conservative kinatarajiwa kumtangaza mshindi wa kinyang’anyiro cha kuongoza chama hicho, kesho Jumatatu na kuhakikisha kwamba kuna waziri mkuu mpya ndani ya muda wa wiki moja.
Waziri mkuu mpya atakuwa wa tatu kuingia ofisi katika kipindi cha mwaka mmoja. Sunak, mwenye umri wa miaka 42, ametangaza kwamba anagombea nafasi hiyo, leo Jumapili. Vyombo vya habari vya Uingereza vinaripoti kwamba anaungwa mkono na wabunge 124 wa chama cha Conservative.
Mshindi anastahili kuungwa mkono na wabunge 100. Mordaunt anaungwa mkono na wabunge 24. Boris Johnson hajatangaza rasmi iwapo anagombea tena kuwa waziri mkuu.