Kura ya maoni Sudan kufikia asilimia 60

  • Mkamiti Kibayasi

Mkazi wa Sudan Kusini katika duka la bidhaa la Nuba. Watu wengi wamejitokeza kupiga kura inayotarajiwa kufikia asilimia 60 inayohitajika kuhalalisha upigaji kura, 11 Jan 2011

Waandaaji wa kura ya maoni juu ya uhuru wa Sudan Kusini wanasema idadi ya wapiga kura waliojitokeza itafika asilimia 60 inayohitajika kuhalalisha upigaji kura.

Mjumbe mmoja wa tume ya kura ya maoni, Suad Ibrahim Eissa, amesema katika taarifa ya Jumatano kwamba idadi ya watu wanaojitokeza itavuka asilimia 60 inayohitajika.

Wapiga kura wamejitokeza kwa idadi kubwa wiki hii katika upigaji kura ambao unatarajiwa kuleta matokeo ya kusini kuamua kujitenga kutoka kaskazini.
Kura ya maoni ya wiki nzima imeingia siku yake ya nne Jumatano na wananchi bado wanajitokeza kupiga kura.

Takribani watu milioni 4 wamejiandikisha kupiga kura. Tume ya kura ya maoni inatarajiwa kutoa matokeo ya awali wiki ijayo.
Wakati huo huo, viongozi kutoka Sudan Kaskazini
na Kusini wanakutana kuzungumzia mapigano ya hivi karibuni katika maeneo ya mpakani yenye mzozo. Mapigano yameuwa watu wasiopungua 46 tangu Ijumaa.

Udhibiti wa eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei ni moja ya masuala kadhaa ya Kaskazini na Kusini lazima yatatuliwe. Viongozi kutoka duniani kote, akiwemo rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, wapo Sudan kushuhudia upigaji kura ya maoni.