Sudan: Mkataba umesainiwa Saudi Arabia, mapigano yanaendelea Khartoum

Moshi ukifuka angani huko kusini mwa jiji la Khartoum wakati mapigano yakiendelea tarehe 6, Mei 2023. Picha na AFP.

Mapigano yameendelea nchini Sudan katika baadhi ya sehemu za mji mkuu Khartoum licha ya kusainiwa makubaliano ya kusitisha vita, katika mazungumzo yanayoongozwa na Marekani, nchini Saudi Arabia.

Makubaliano hayo yameongeza matumiani ya kusitisha vita hivyo ambavyo vimeingia wiki ya tano.

Makubaliano yaliyosainiwa kati ya wawakilishi wa jeshi la serikali na wapiganaji wa kikosi cha dharura cha RSF, baada ya kufanyika mazungumzo mjini Jeddah, Saudi Arabia, yanatarajiwa kuanza kutekelezwa Jumatatu jioni kwa uangalizi wa mkakati wa kimataifa.

Makubaliano hayo yanaruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu ambao wameathiriwa na vita hivyo.

Makubaliano ya kila mara ya kusitisha mapigano yaliyoanza April 15, yamekuwa hayaheshimiwi, lakini yale ambayo yamesainiwa mjini Jeddah ndiyo ya kwanza kupatikana baada ya mazungumzo.

Wachambuzi wanasema kwamba hakuna ishara kwamba kiongozi wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na kiongozi wa kikosi maalum cha jeshi Mohamed Hamdan Dagalo, maarufu Hemedti, wanaweza kutekeleza makubaliano ya kusitisha vita kwa sababu wote wameashiria kwamba wapo tayari kupigana hadi wapate ushindi.