Sudan Kusini yashutumiwa kuwabaka wasichana na wanawake

Antonia Mulvey ni mkurugenzi wa Legal Action Worldwide anadai jeshi la Sudan Kusini lilitenda manyanyaso ya kikatili ya ngono ikiwemo utumwa wa ngono, mateso ya ngono na ubakaji wa genge dhidi ya wanawake na wasichana

Kundi moja la wanasheria wa haki za binadamu limefungua mashtaka dhidi ya serikali ya Sudan Kusini kwa manyanyaso ya ngono kwa niaba ya wanawake na wasichana 30 wa Sudan Kusini ambao wanadaiwa walibakwa na wanajeshi wa Sudan Kusini pamoja na walinzi wa rais.

Antonia Mulvey ni mkurugenzi wa Legal Action Worldwide-LAW mtandao usio wa kiserikali wa mawakili wa haki za binadamu anadai jeshi la Sudan Kusini lilitenda manyanyaso ya kikatili ya ngono ikiwemo utumwa wa ngono, mateso ya ngono na ubakaji wa genge dhidi ya wanawake na wasichana.

Antonia Mulvey

Mulvey alisema malalamiko yaliwasilishwa Alhamis mjini Geneva kwenye kamati ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake-CEDAW. Aliendelea kusema kwamba kamati hiyo itatathmini malalamiko na nakala yake itapelekwa kwa serikali ya Sudan kusini kutoa majibu.

Pia alisema kwa sababu ya mashtaka yenyewe tunalinda wajihi wa walionusurika na visa hivyo ambapo tunatumia majina yao ya kwanza pekee. Kwa mujibu wa taarifa ya LAW wanawake na wasichana 30 ambao wapo katika kambi za wakimbizi nchini Uganda ni pamoja na msichana wa miaka 12 ambaye alishuhudia dada zake wawili pamoja na jirani wakibakwa baada ya yeye kufanyiwa ukatili huo wa kubakwa.