Sudan Kusini imeanza tena kuchimba mafuta

Vitalu vya mafuta vya Toma, jimbo la Ruweng state, Sudan kusini. Aug. 25, 2018.

Sudan Kusini inapanga kuanza tena uchimbaji mafuta ghafi baada ya mapigano yanayoendelea katika nchi jirani ya Sudan kusababisha uharibifu kwenye bomba la kusafirisha mafuta mapema mwaka huu.

Sudan Kusini, yenye idadi kubwa ya watu maskini imekuwa ikisafirisha mafuta yake kwenda kwenye soko la kimataifa kupitia Port Sudan katika Bahari ya Sham, na kuilipa Sudan gharama ya usafirishaji huo.

Lakini bomba la mafuta liliharibiwa mwezi Februari katika mapigano kati ya kikosi cha dharura cha RSF na jeshi la Sudan, hatua ambayo iliepelekea Sudan Kusini kukabiliwa na hali mbaya ya uchumi.

Barua iliyoandikwa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya mafuta Sudan Kusini Kon John Akot inasema kwamba wizara ya mafuta ya Sudan Kusini imetangaza kuanza tena uchimbaji mafuta kuanzia Jumatatu Desemba 30, 2024.

Kabla ya bomba hilo kuharibiwa, Sudan Kusini ilikuwa ikizalisha zaidi ya mapipa 150,000 ya mafuta ghafi kila siku.