Sri Lanka yapata rais mpya

Rais mpya wa Sri Lanka, Ranil Wickremesinghe

Bunge la Sri Lanka Jumatano limemchagua waziri mkuu Ranil Wickremesinghe, kuwa rais wa taifa hilo linalopitia misukosuko.

Akiwa na umri wa miaka 73, Wickremesinghe alipata kura 134 katika bunge lenye wabunge 225 katika kura zilizopigwa leo, ambapo kura 82 zilikwenda kwa Dullas Alahapperuma, mwanahabari wa zamani ambaye alishikilia wizara mbalimbali za serekali katika chama tawala cha SLPP.

Anura Dissanayake, kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto JVP, alipata kura tatu tu.

Kura hizo zimepigwa ikiwa ni wiki moja baada ya aliyekuwa rais Gotabaya Rajapaksa kukimbia Sri Lanka, baada ya vuguvugu na ghasia zilizo sababishwa na hali ngumu ya uchumi ya miezi kadhaa iliyofanya nchi kushindwa kuagiza chakula, mafuta ama dawa kutokana na kuisha kwa hifadhi ya fedha za kigeni.