Katika taarifa yake Pelosi amesema yeye na wabunge wengine watano wa chama cha Democrat wanakusudia kuthibitisha dhamira thabiti na isiyoweza kutetereka ya Marekani kwa washirika wao na marafiki katika eneo hilo.
Taarifa imeongeza kusema kuwa, ziara hiyo itahusisha kusimama Singapore, Malaysia, Korea kusini, na Japan .
Kundi hilo tayari limesimama Hawaii ambako limepokea maelezo kutoka Komand ya Indo- Pacific ya jeshi la Marekani.
Ripoti ya vyombo vya habari vya Marekani Ijumaa vilionesha kwamba Pelosi alikuwa anapanga bila kuwa na uhakika kusimama Taiwan.
Hata hivyo spika mwenyewe alizungumza kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja kuhusu uwezekano huo, licha ya kwamba ofisi yake haijathibitisha kutokana na taratibu za kiusalama.
Hii itakuwa ziara ya hali ya juu ya maafisa wa Marekani kutembelea Taiwan tangu mwaka 1997 wakati spika wa bunge wa zamani Newt Gingrich alipoongoza ujumbe wa bunge huko.