Spika wa Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani aondolewa

Mbunge Kevin McCarthy akiondoka katika ukumbi wa Bunge baada ya kuondolewa kama Spika wa Bunge mjini Washington Dc Jumanne, Oktoba 3, 2023

Wabunge 8 wa chama cha Republican walipiga kura pamoja na Wademokrat wote waliokuwepo kumwondoa McCarthy, ambaye atabaki kuwa mbunge licha ya kuondolewa kwake kutoka ofisi ya spika.

Baraza la wawakilishi la bunge la Marekani limepiga kura ya kumuondoa madarakani Spika Kevin McCarthy kama kiongozi siku ya Jumanne, na kumfanya kuwa spika wa kwanza katika historia ya Marekani kuwahi kuondolewa baada ya siku 269 tu kwenye usukani, kufuatia uasi kati ya wabunge wa siasa kali za mrengo wa kulia ambao wanahudumu ikiwa ni mfano wa migawanyiko mikubwa ndani ya Chama cha Republican.

Wabunge 8 wa chama cha Republican Matt Gaetz, Andy Biggs , Ken Buck, Tim Burchett , Eli Crane , Bob Good , Nancy Mace na Matt Rosendale walipiga kura pamoja na Wademokrat wote waliokuwepo kumwondoa McCarthy, ambaye atabaki kuwa mbunge licha ya kuondolewa kwake katika ofisi ya spika.

Mbunge Patrick McHenry Mrepublikan anachukua nafasi ya McCarthy kama spika wa muda kwa mujibu wa kanuni za Bunge ambazo zilimtaka McCarthy kutoa orodha ya watakaochukua nafasi za muda iwapo nafasi itakuwa wazi.

Kura hiyo rasmi inafuatia juhudi zilizofeli za McCarthy na washirika wake mapema Jumanne kuwasilisha azimio la kumuondoa madarakani, wakati Warepublican 11 walipiga kura pamoja na wademokrat kusonga mbele na kura ya kumuondoa.

KILICHOTOKEA

Mbunge Matt Gaetz alianzisha hoja ya kumuondoa spika Jumatatu jioni baada ya Kevin McCarthy kushirikiana na Wademokrat kupitisha mpango wa matumizi kwa siku 45 ili kuzuia kufungwa kwa serikali. Gaetz alipinga vikali mpango wowote wa matumizi ya muda mfupi na alimshutumu spika McCarthy kwa kujadili mpango wa siri ili kutoa ufadhili zaidi kwa Ukraine, ingawa ufadhili wa Ukraine uliondolewa kwenye bajeti ya muda katika jitihada za kuvutia kura za kutosha za Republican kuipitisha.

McCarthy alichaguliwa kuwa spika wa bunge mwezi Januari kufuatia duru 15 za upigaji kura, ikiwa ni mara ya kwanza tangu 1860 uchaguzi wa uspika kuchukua awamu tisa.

Alishinda tu baada ya kukubaliana na msururu wa makubaliano na watetezi wake wa mrengo wa kulia, akiwemo Gaetz, ambao alimtaka kubadili sheria za Bunge ili kuruhusu mjumbe mmoja tu kuleta hoja ya kuondolewa.

Migawanyiko mikubwa ndani ya Chama cha Republikan ilizuia mara kwa mara uwezo wa McCarthy kutayarisha mikutano ya Warepublican huku wanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia walipopata wingi wa kura 222 kwa 213 katika Bunge ili kushinikiza madai yao badala ya kura katika masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na mpango wa ukomo wa deni mwezi Juni na. mazungumzo ya hivi karibuni ya bajeti.