Jeshi la Sudan Kusini linadai kuwa Jumatano liliteka mji muhimu uliokuwa ukishikiliwa na waasi - Leer - katika jimbo la Unity lenye utajiri wa mafuta.
Jimbo hilo ni mahali alikozaliwa Makamu Rais aliyegeuka kuwa kiongozi wa waasi Riek Machar na kukamatwa kwake kumetokea baada ya mapigano makali kuliko yote katika mgogoro huo wa miezi 17 sasa.
Msemaji wa jeshi Kanali Philip Aguer alisema jeshi la serikali SPLA linashikilia pia mji wa Palouch kinyume na madai ya waasi kuwa wameteka mji huo na visima vyake vya mafuta.
"Wilaya pekee ambayo bado iko mikononi mwa waasi ni Panyijiar. Majeshi ya SPLA yako Leer na zaidi ya asilimia 95 ya jimbo la Unity liko chini ya udhibiti wa SPLA usiku huu," alisema msemaji huyo.
Aguer alielezea madai ya waasi ya kudhibiti Palouch kama ushindi wa "muda mfupi."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon Jumatano alikemea mapigano hayo mapya akisema ni ukiukaji mwingine wa mkataba wa kusitisha mapigano wa January 2014.