Makundi ya misaada Afrika Kusini yanasema zaidi ya raia wa kigeni 2,000 wako katika kambi za wakimbizi katika mji wa pwani wa Durban kufuatia mashambulizi yanayofanywa dhidi ya wahamiaji nchini humo.
Imtiaaz Sooliman, wa kundi la Gift of the Givers, alisema Jumatano kuwa kambi hizo katika viwanja vya michezo mjini humo hazitatosha endapo ghasia hizo zitaendelea.
Msemaji wa polisi Kanali Jay Naicker alisema watu 74 wamekamatwa baada ya watu watano kuuawa katika mashambulizi hayo.
Magazeti ya Afrika Kusini yamechapisha picha za raia wa kigeni wakiwa wamejihami kwa visu na mapanga kujilinda. Gazeti la Star limesema wenye maduka wa Kinigeria walijizingira kwa matairi yaliyowashwa moto wakati Waafrika Kusini wakipora vitu katika maduka yao.
Mjini Johannesburg, ambako waporaji walivamia maduka yanayomilikiwa na wageni mapema mwaka huu, wahamiaji walifunga maduka yao kupeka uwezekano wa ghasia.