Wakizungumza na Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Amerika wanaharakati hao wamesema kutokuwepo na utaratibu wa kukusanya vifaa hivyo kunasababisha kusambaa kwa chupa za plastiki pamoja na vifaa vya elekroniki zikiwemo simu na komputa ambazo husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Patrick Kipalu mkurugenzi wa mipango ya Afrika katika Mradi wa Haki na Rasilimali (RPR) ambao ni muungano wa mashirika ya kutetea haki za ardhi za jamii katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, anasema makampuni yanayotengeneza bidhaa hizi lakima yawajibike kugharamia ukusanyaji na uchakataji wa mabaki ya bidhaa zao zinazouzwa barani Afrika.
Amesema mara nyingi miradi ya uchakataji ina gharama kubwa na serikali hazitoi fedha kuendesha miradi hiyo, “kwa hiyo makampuni yanayotengeneza bidhaa hizo yanapaswa kulipia gharama hizo za ukusanyaji na uchakataji,”aliongeza.
Aidha wanaharakati hao walisema chupa za plastiki na vifaa vya elekroniki vinapoharibika vimekuwa vikitupwa katika majalala kwa sababu ya ukosefu wa mfumo wa ukusanyaji na uchakataji.
“Wakati mwingine simu ikiharibika na ikishindikana kutengenezeka huwa namwachia fundi, lakini mara nyingi huwa nawaachia watoto wanachezea, wakiivunja inakuwa hatari ndipo naitupa jalalani,” alisema Mithle Aromo mkazi wa Dar Es Salaam.
Mwenyekiti wa klabu ya Mazingira ya Green awareness Club yenye makao mjini Arusha, Tanzania, Ibrahim Sinsakala anasema yeye binafsi simu inaposhindika kutengenezeka humuachia fundi. ambaye “hutoa vipuri ambavyo huviuza na kutupa mabaki.”
Katika mji wa Kampala, viwanda vya uchakataji havikidhi mahitaji ya jiji na hivyo kuwalazimu watu kutupa kiholela bidhaa hizo , alisema Omona Andrew David mkazi wa jiji hilo.
Baadhi ya wanaharakati hao wanalazimika kurundika vifaa vyao vya kielekroniki ndani ya nyumba au maofisini wakihofia usalama wa taarifa zao zilizopo katika simu na kompyuta na vifaa vingine wakati ya uchakataji.
MARIAM MNIGA, SAUTI YA AMERIKA, WASHINGTON DC.