Kauli mbiu ya mwaka huu kuadhimisha siku ya Umoja wa Afrika ni kuhamasisha kuwawezesha vijana kwa ajili ya maendeleo endelevu. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anadhimisha siku hiyo kwa kuzuru bara hilo kwa lengo la kuhimiza juhudi za mikamatifa kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema sherehe za mwaka huu zinafanyika wakati waafrika wengi wanasimama na kudai uhuru wa kweli, utawala bora na kulaani ulaji rushwa.
Akizungumza na Sauti ya Amerika Dk. Bashiru Aly, wa chuo kikuu cha Dar es salam anasema kinachohitajika hivi sasa ni kwa waafrika kurudi mahala walipoanzia kupigania uhuru. "Uhuru wa Afrika ulipatikana kutokana na kujitoa mhanga, na kuwa na uwongozi shupavu lakini pia kuwa na dhamira ya kutafuta maendeleo kwa pamoja. Afrika kama hiajaungana haina mustakbali mwema, mustakbali mwema unategemea umoja ndani ya nchi za Afrika lakini zaidi baina ya nchi za Afrika".