Aidha, rais huyo alitangaza marufuku ya abiria kutoka nchi zote ambako visa vya Coronavirus vimeripotiwa kufikia sasa.
Kenyatta alitangaza hayo alipowahutubia waandishi wa habari mjini Nairobi baada ya kuthibitishwa kwa visa vingine viwili vya maambukizi ya Covid-19.
Maafisa wa wizara ya Afya walithibitisha kwamba watu hao wawili walikuwa wametangamana na mgonjwa wa kwanza.
"Wote ni raia wa Kenya. Mmoja ana uraia pacha wa Kenya na Uingereza," alisema waziri wa Afya Mutahi Kagwe.
Siku ya Alhamisi, Kenya iliripoti kisa cha kwanza cha Coronavirus cha mwanamke mwenye umri wa miaka 27 ambaye alikuwa amesafiri kutoka jimbo la Ohio, Marekani.
Mwanamke huyo anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Kenyatta mjini Nairobi.
Kenyatta alitangaza kufungwa kwa shule zote zisiizo za malazi kuanzia Jumatatu huku wanafunzi wote wanaolala shuleni wakitakiwa kuondoka na kwenda manyumbani mwao kuanzia Jumanne.
Alisema vyuo vikuu vimepewa hadi Ijumaa kufunga.
USAFIRI
Rais Kenyatta alisema raia wa Kenya bado wanaweza kuingia nchini kwa masharti kwamba watawekwa kwenye karantini kwa kipindi cha siku 14 baada ya kuwasili nchini.
Aidha, aliwaonya wafanyabiashara dhidi ya ulaghai wa kuongeza bei za bidhaa kinyume cha kanuni na sheria.
"Iwapo wafanyabiashara watawalaghai raia wa kawaida, watachukuliwa hatua kali," aliongeza.