Shughuli ya kuwahamisha raia zaidi kutoka katika kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa bandari wa Mariupol uliozingirwa nchini Ukraine imeanza.
"Hatua inayofuata ya kuwaokoa watu wetu kutoka Azovstal inaendelea kwa sasa," Andriy Yermak, mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Ukraine, alisema leo Ijumaa.
Kulikuwa na maelezo machache, hata hivyo, kuhusu operesheni hiyo. "Taarifa kuhusu matokeo itatolewa baadaye," Andriy alisema.
Siku ya Alhamisi, mapigano yalizuka katika kituo hicho, lakini wapiganaji wa Ukraine waliendelea kupambana huku wanajeshi wa Russia wakiingia ndani ya jengo hilo licha ya ahadi ya Russia ya kusitisha mapigano wakati wa mchana ili kuruhusu zaidi ya raia 200 waliokwama katika kituo hicho kuhamishwa salama.