MCT yapinga sheria inayokandamiza uhuru habari Tanzania

Katibu Mkuu wa chama cha waandishi habari Tanzania Neil Meena akizungumzia usalama wa waandishi.

Wadau wa habari wakiongozwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) leo Jumatano wamefungua kesi ya kupinga sheria ya huduma za vyombo vya habari namba 12 ya mwaka 2016 katika mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) jijini Dar es salaam.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili; ya VOA, Dina Chahali ameripoti kuwa Katibu mtendaji MCT, Kajubi Mukajanga aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kufungua kesi hiyo kuwa sheria hiyo inafinya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

“Uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa demokrasia ya utawala wa sheria, uwajibikaji, uwazi na utawala bora…,”alisema Mukajanga.

Amesema Tanzania iliridhia mkataba huo wa Afrika Mashariki, Julai 7, 2000 chini ya kifungu cha 23 cha mkataba huo.

“Mahakama hii tuliyofungua kesi imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huu na kuhakikisha nchi wanachama wanaufuata na kuusimamia,” amesema katibu mtendaji.

Mwandishi wa VOA ameongeza kuwa wadau wengine wa habari na watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania nao wameungana na Baraza la habari Tanzania katika kufungua kesi hiyo ya kupinga sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016.

Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu, Helen Kijo Bisimba ameelezea pia kuguswa na sheria hiyo ambayo anasema inakiuka haki za binadamu.

Mwanahabari mkongwe Jenerali Ulimwengu ni miongoni mwa watakaosimamia kesi hiyo.
Hivi sasa wadau mbalimbali wa habari nchini wamekamilisha kupeleka mapendekezo ya kanuni za sheria hiyo ya huduma za vyombo vya habari ambazo ziko chini ya mamlaka ya waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Nape Nnauye.