Pompeo aitaka Iran kutekeleza masharti kuwa rafiki wa Marekani

Mazungumzo yaliyojiri kati ya serikali ya Iran na shirika la IAEA, Umoja wa Ulaya nchini Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema iwapo viongozi wa Iran watakubali matakwa ya Marekani kwamba wafanye shughuli zao kama taifa jingine la kawaida, Marekani itaitembelea Iran na kuifanya kuwa rafiki yake.

Katika mahojiano maalum na VOA Ijumaa, Pompeo amesema lengo la mkakati mpya juu ya Iran ambao alilieleza mapema wiki hii ni kuweka masharti kwa viongozi wenye msimamo wa Kiislam Iran kuendesha shughuli zao kama “viongozi wa kawaida.”

Akizungumza na VOA katika Wizara ya Mambo ya Nje Ijumaa, amesema viongozi wa “kawaida” hawawaibii wananchi wao au kufuja fedha zao kwa “majaribio” nchini Syria na Yemen, kama alivyoliweka hilo.

Kama tunaweza kuweka masharti ambapo [viongozi wa Iran] wataacha [tabia hiyo], wananchi wa Iran watakuwa na mafanikio makubwa, na watatembelewa na Wamarekani, na tutaweza kuwa na mambo makubwa tunayoyafanya kunapokuwa na marafiki na washiriki wetu,” amesema Pompeo.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu ameeleza juu ya masharti 12 ya mkakati wake alioutoa katika hotuba yake kwa kusema Iran lazima waruhusu Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic (IAEA) kukagua maeneo yake ya kijeshi na maabara ya tafiti.

Katika hotuba yake ya Mei 21, alitoa wito kuwa IAEA ipewe ruhusa bila masharti kukagua maeneo yote nchi nzima.

Pompeo pia ameongeza kuwa Marekani inataka Iran iache kabisa vitisho vyake vya kuiangamiza Israel na kuacha tabia zake nyengine za vitisho kwa majirani zake.

Amesema viongozi wa Iran sio tu kwamba wanalazimika kuacha kuwahamasishawananchi kuendelea kushinikiza kauli yao ya “ Maangamizi kwa Israel” lakini kauli nyingine ya "Maangamizi kwa Marekani,”

Pompeo amesisitiza kuwa Marekani haitaki kuleta mapinduzi Iran na amevishauri vikundi vya upinzani vya Iran kutofanya hilo pia. “Hatutaki wahamasishe suala la kupindua serikali,” amesema.

Amesema muda wa kuwa vikundi hivi vinafanya shughuli zake kwa malengo yaliyowekwa na Marekani, tunaunga mkono juhudi zao.