Shambulizi linaloshukiwa kuwa la kigaidi latokea Nairobi, Kenya

Shambulizi katika eneo la Chiromo, Riverside Drive, Nairobi, Kenya

Mlipuko uliofuatiwa na milio ya risasi ulishuhudiwa katika hoteli ya Dusit katika eneo la Chiromo, mjini Nairobi, katika kile ambacho vyombo ya habari vya Kenya vinashuku kuwa ni shambulizi la kigaidi.

Maafisa wa polisi waliendelea kuwasili katika eneo hilo kwenye barabara ya Riverside Drive.

Polisi walisema kuwa watu kadhaa walijeruhiwa na walihudumiwa na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakisaidiana na watu wengine wa kujitolea.

Baadhi ya majeruhi walipelekwa kwenye hospitali mbalimbali ambako wanaendelea kupokea matibabu.

Tukio hilo la mwendo wa saa 3.15 alasiri, lilisababisha msongamano mkubwa kwenye barabara za eneo hilo.

Jumba hilo, ambalo lina hoteli ya kifahari na afisi za kampuni mbalimbali, lilionekana kuzingirwa na maafisa wa kulinda usalama.

Shirika la habari la Al-Jazeera liliripoti kwamba kundi la kigaidi la Boko Haram lilidai kuhusika katika shambulizi hilo.

Haya yalitokea siku moja tu baada ya mahakama moja jijini Nairobi kuwapata na hatia watu watatu wanaotuhumiwa kupanga shambulizi la kigaidi katika jumba la kibiashara la West Gate miaka sita iliyopita na kumuachilia mshukiwa mmoja kile ilichokitaja kuwa kutokuwepo kwa ushahidi,

Punde tu baada ya shambulizi hilo la Jumanne, moshi, milio ya risasi na milipuko miwili ilisikika jioni katika jengo la Du sit Du 2 katika eneo la Riverside jijini Nairobi dakika chache kabla ya saa kumi jioni.

Jumbe mbalimbali za usaidizi zilisambaa katika mitandao ya kijamii nchini Kenya yakiwa ni maandishi ya baadhi ya raia wa Kenya wanaotaka usaidizi kutoka jengo hilo ambalo lina mighahawa na afisi.

Katika mapeperusho ya mbashara, runinga za Kenya zilionyesha yaliokuwa yakitukia pembeni mwa jengo hilo huku manusra wengi wakitolewa na vyombo vya usalama. Huku waokoaji wa shirika la msalamba mwekundu wakiwa mbioni kuwaondoa watu waliokwama katika jengo hilo.

Moshi mzito mweusi uligeuza anga kutoka eneo la uegeshaji huku magari yakiteketea kwa moto na watu wengine wengi wakiondoka kwa haraka kutoka jengo hilo.

Shambulizi hilo ambalo maafisa wa polisi wanakisia kuwa huenda likawa la kigaidi, na ishara zikionesha hivyo, linajiri katika maadhimisho ya miaka mitatu baada ya tukio la kigaidi la El Adde kwenye kambi ya wanajeshi wa Kenya nchini Somalia ambapo wanajeshi wengi wa Kenya waliuawa.

Msemaji wa serikali ya Kenya Erick Kiraithe, ameiambia idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kuwa vyombo vya usalama vinaendelea kudhibiti mashambulizi ya aina yoyote.

Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet, ameviambia vyombo vya habari kuwa vyombo vya usalama vinakisia kuwa shambulizi hilo ni la kigaidi.

Aidha, Bw Boinnet ameeleza kuwa vyombo vya usalama kutoka vitengo tofauti tofauti vinaendelea kudhibiti mashambulizi zaidi huku uokoaji ukiendelea.

Hata hivyo ametoa masikitiko yake kwa kuwepo majeraha ambayo ameeeleza idara husika itatoa taarifa kamili.

Mpaka tukienda hewani, shughuli za uokoaji zinaendelea katika jumba hilo na japo sasa milio ya risasi imekoma kwa kipindi kingi, maafisa wa polisi wanaendelea kuongeza jitihada kuendeleza uokoaji.

Mwaka 2013, wanamgambo wa Alshabaab walilivamia jengo la kibiashara la West Gate na kuwaua watu zaidi ya sitini na kuwajeruhi wengine zaidi. Vile vile 2015, wanamgambo hao walikivamia chuo kikuu cha Garissa mashariki ya Kenya na kuwaua wanafunzi zaidi ya mia moja.

-Mwandishi wa Sauti ya Amerika, Kennedy Wandera, amechangia ripoti hii.