Shambulizi la kombora la Israel lauwa watu 19 katika Ukanda wa kusini mwa Gaza

  • VOA News

Wapalestina wakagua uharibifu wa shambulizi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Masawi, Khan Yunis, Ukanda wa kusini mwa Gaza, Septemba 10, 2024. Picha ya AFP

Wizara ya afya huko Gaza Jumanne ilisema shambulizi la kombora la Israel katika eneo lililotengwa kuhifadhi wakimbizi wa ndani katika Ukanda wa kusini mwa Gaza, liliua watu 19 na kujeruhi wengine 60.

Wizara hiyo ilisema waokoaji walikuwa hawajaweza kufika kwenye eneo la tukio ili kuwaondoa baadhi ya waathirika waliofukiwa chini ya mchanga na vifusi.

Idadi hiyo ya vifo ni ndogo kuliko iliyokuwa imetolewa awali na idara ya ulinzi wa raia, ambayo ilisema watu 40 waliuawa.

Jeshi la Israel limepinga idadi hiyo kubwa ya vifo, likiishtumu Hamas kwa kuendesha operesheni yake katika maeneo kunakoishi wakimbizi wa ndani.

Shambulizi hilo lilifanyika huko Mawasi, magharibi mwa mji wa Khan Younis, ambako jeshi la Israel liliwambia maelfu ya Wapalestina kuondoka.

Jeshi la Israel limesema lilishambulia wanamgambo kadhaa wakuu wa Hamas, wakiwemo makamanda kadhaa ambao walihusika moja kwa moja katika shambulizi la Oktoba 7 dhidi ya Israel ambalo lilichochea vita.