Shambulizi la kigaidi Kenya :Mbwa maalum watumiwa kutafuta mabomu

Ndugu wa mmoja wa wale walioathiriwa na shambulizi la kigaidi akisindikizwa na wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu akiwa na majonzi baada ya kwenda kwenye chumba cha kuhifadhi maiti jijini Nairobi, Kenya Alhamisi, Jan. 17, 2019.

Wakati taarifa za mmoja wa washambuliaji katika tukio la kigaidi ambaye aliwauwa watu 21 zikitolewa, majeshi ya usalama ya Kenya Alhamisi yanaendesha tena msako kwenye eneo la tukio wakitumia mbwa maalum wenye uwezo wa kugundua mabomu.

Pia watalaam wa mabomu wanaendelea kupekuwa hoteli ya DusitD2 na maeneo ya ofisi mbalimbali Alhamisi ambako shambulizi la kigaidi lilfanyika jijini Nairobi.

Chanzo cha habari katika jeshi la polisi nchini Kenya ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwa sharti ya kuwa jina lake lihifadhiwe, kuwa walikuwa na uhakika kuwa hakuna watu waliokwama hapo hotelini au katika majumba yanayo zunguka majengo ya ofisi baada ya shambulizi la masaa 20, ambapo raia 700 waliokolewa.

Amesema katika hali kama hii, haiwezi kukufanya upumzike mpaka uangalie kila kitu. Tumerejea na mbwa maalum na watalaamu wa mabomu ambao wanakagua kila sehemu kwa sababu tumegundua kuna magruneti ambayo yaliachwa nyuma na washambuliaji hao.

Polisi wameuonya umma huenda wakasikia milio mikubwa ya milipuko wakati wakiendelea na ukaguzi huo kwenye hoteli hiyo.

Watu watano walio kuwa na bunduki wa kundi la wanamgambo la Al–Shabaab lenye uhusiano na Al Qaida waliishambulia hoteli ya DusitD2 na maeneo ya ofisi Jumanne mchana.