Shambulizi katika kliniki moja kaskazini mwa Gaza lajeruhi  watu sita :Maafisa wa Palestina

Mwanaume mmoja wa Kipalestina akiwa amepanda mkokoteni wa kuvutwa na farasi, karibu na jengo lililoharibiwa ambapo mali za watu binafsi na magari yamebanwa kati ya tabaka za vifusi katika Jiji la Gaza Novemba 2, 2024.

Maafisa wa Palestina wanasema shambulizi la ndege zisizo na rubani za Israel katika kliniki moja kaskazini mwa Gaza ambako watoto walikuwa wakipatiwa chanjo ya polio lilijeruhi  watu sita wakiwemo watoto wanne. Lakini Jeshi la Israel lilikanusha kuhusika.

Shambulio hilo lilitokea Jumamosi kaskazini mwa Gaza, ambayo imezingirwa na vikosi vya Israel na kwa kiasi kikubwa imetengwa kwa mwaka mmoja uliopita. Israel imekuwa ikifanya mashambulizi mengine huko katika wiki za hivi karibuni ambayo yameuwa mamia ya watu na kusababisha maelfu kuyahama makazi yao.

Haikuwezekana kuweka sawa ushahidi unaopingana . Wanajeshi wa Israel wamevamia mara kwa mara hospitali za Gaza katika kipindi cha vita, wakisema Hamas inazitumia kwa malengo ya kigaidi, madai ambayo yamekanushwa na maafisa wa afya wa Palestina.

Dk. Munir al-Boursh, mkurugenzi mkuu wa Wizara ya Afya ya Gaza, aliliambia Shirika la Habari la Associated Press kwamba ndege isiyo na rubani ilipiga kliniki ya Sheikh Radwan katika Jiji la Gaza mapema Jumamosi mchana, dakika chache tu baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuondoka kwenye kituo hicho.

Shirika la Afya Duniani na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la UNICEF, ambao kwa pamoja wanafanya kampeni ya chanjo ya polio, walielezea wasiwasi wao juu ya taarifa za shambulizi hilo.