Watu wenye silaha waliuwa watu wasiopungua 14 Jumanne katika shambulizi moja kwenye kijiji kilichopo kaskazini-mashariki mwa Kenya.
Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya lilisema watu wasiopungua 11 wengine walijeruhiwa katika shambulizi hilo katika kijiji cha Soko Mbuzi linalopakana karibu na mpaka wa Kenya na Somalia. Maafisa walisema waathirika wa shambulizi hilo walikuwa wafanyakazi katika mgodi wa mawe.
Kundi la wanamgambo wa al-Shabaab lenye makao makuu yake Somalia limefanya mashambulizi kadhaa nchini Kenya tangu jeshi la Kenya lilipojiunga katika juhudi za kupambana na wapiganaji wenye uhusiano na al-Qaida huko nchini Somalia mwaka 2011.
Mashambulizi hayo yanajumuisha matukio kadhaa makubwa ikiwemo wanamgambo wa kundi hilo kuuwa watu 148 kwenye chuo kikuu cha Garissa hapo mwezi April na kuuwa watu wasiopungua 67 kwenye eneo lenye maduka mengi ya kifahari la Westgate Mall mjini Nairobi mwaka 2013.
Wakati huo huo Seneta wa mji wa Mandera, Billow Aden Kerrow aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba shambulizi hilo limefanywa na kundi la al-Shabab. Vyombo vya habari vinavyounga mkono kundi hilo nchini Somalia pia vinaripoti kwamba kundi hilo ndilo lililofanya shambulizi hilo.
Bwana Kerrow alisema shambulizi lililenga nyumba mbili zinazokaliwa na Wakenya wasio wasomali ambao wanafanya kazi ya ujenzi na biashara nyingine. Alisema kuwa shambulizi lilihusisha watu wenye silaha wapatao 20.