Shambulio la kombora la Russia laua watu 7 katika mji wa kihistoria wa Ukraine

Kanisa kuu la mji wa Ukraine wa Odesa lililoharibiwa na shambulio la kombora la Russia, Julai 23, 2023

Watu saba akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 6 waliuawa na wengine 90 kujeruhiwa wakati kombora la Russia lilipopiga eneo la katikati mwa mji wa kihistoria wa Chernihiv kaskazini mwa Ukraine, wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine imesema Jumamosi.

Watu walikuwa wanaelekea kanisani kusherekea siku kuu ya kidini wakati shambulio hilo lilipofanyika, wizara hiyo imesema, ikiongeza kuwa watu 12 kati ya waliojeruhiwa ni watoto na 10 ni maafisa wa polisi.

“Kombora la Russia lilirushwa katikati mwa mji, katika Chernihiv yetu. Eneo la chuo kikuu cha sayansi ya ufundi, ukumbi wa michezo ya kuigiza,” Rais Volodymyr Zelenskiy aliandika kwenye mtandao wa Telegram akiwa katika ziara ya kikazi nchini Sweden.

Video fupi inayoambatana na ujumbe wa Zelenskiy imeonyesha mabaki ya vifusi vilivyosambaa katika eneo hilo mbele ya jengo la michezo ya kuigiza, ambako magari yaliyokuwa yameegeshwa hapo yaliharibiwa vibaya.

Video hiyo pia kwa ufupi iliuonyesha mwili uliokuwa ndani ya gari.