Shahidi amkana Tido Mhando kesi ya matumizi mabaya ya madaraka

Tido mhando

MKURUGENZI Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Clement Mshana, amedai mahakamani kwamba Mei 28, 2012 alishangaa kupokea taarifa ya usuluhishi kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1) ya Uingereza kwa madai ya kuisababishia hasara.

Mshana alitoa madai hayo Ijumaa wakati akitoa ushahidi dhidi ya mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Tido Mhando, anayekabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka ikiwamo kuisababishia serikali hasara ya Sh. Milioni 887.1.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe nchini Tanzania, wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Leonard Swai, shahidi huyo alidai kuwa kampuni hiyo iliwaahidi kuwapatia kazi ya kuhamisha urushaji wa matangazo kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali katika televisheni.

Mshana ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2011 hadi 2016 alidai kuwa alishangaa na kushtuka kwa sababu walipelekewa madai ya pesa nyingi na walipewa siku 28 kuwa lazima TBC iwe imejibu madai hayo.

Alidai kuwa aliwasiliana na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TBC iwapo analifahamu suala hilo au waliwahi kutoa baraka kwa sababu ndio wasimamizi wakuu wa shirika.

Hata hivyo, alidai kuwa mwenyekiti wa bodi alieleza kwamba hakufahamu mkataba huo ulioingiwa kati ya Tido na Channel 2 Group Corporation (BV1).

"Mwenyekiti wa bodi alinielekeza niandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo labda analifahamu suala hilo...Wizara ya Habari, ilimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuliangalia hilo suala na kutoa ushauri wa kisheria na maelekezo"alidai shahidi na kuongeza.

"Katika kumbukumbu zangu Wizara ilitoa maelekezo kwa bodi ya wakurugenzi ya TBC iitishe kikao cha kujadili na kutoa mapendekezo kwa sababu ilitaka kujua zaidi kuhusu mkataba huo...mbali na wizara na AG, Msajili wa Hazina naye alifahamishwa kwa sababu yeye ndiye amepewa dhamana na mali za shirika pamoja na Wizara ya Fedha ambayo ni mtoa fedha," alidai Mshana.

Alidai kuwa katika taarifa ya usuluhishi aliyoipokea, Channel 2 Group Corporation ilidai kuwa TBC imewasababishia kukosa faida ambayo wangeipata iwapo wangewekeza katika kuhamisha urushaji wa matangazo ya televisheni kutoka mfumo wa analojia kwenda digital.