Serikali ya Mexico yaendelea na juhudi za kuwatafuta wanusurika wa tetemeko

Wananchi wakisaidiana kumuondoa mtu aliyejeruhiwa katika tetemeko la ardhi Mexico City

Waokoaji wameendelea Jumatano kufukua vifusi baada ya tetemeko la Mexico City na majimbo yaliyokaribu kwa matumaini ya kuwakuta walionusurika katika tetemeko la ardhi.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.1 wa kipimo cha 'ritcher scale' limewaua watu wasiopungua 225 na kuangusha dazeni za majumba.

Waziri wa Mambo ya Ndani Miguel Osorio Chong amesema vikosi vya jeshi la Mexico na polis wataendelea na zoezi la kuwatafuta watu waliofunikwa na kifusi mapaka wahakikishe kuwa kila mbinu ya kuwapata watu hao wakiwa hai imetumika kikamilifu.

Raia pia waliungana na timu za waokoaji muda mfupi baada ya tetemeko hilo kutokea Jumanne, wakitumia machine kubwa za kuchimbua na mikono yao kuondoa vifusi vilivyokuwa vimerundikana.

Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa eneo la Puebla, kilomita 123 kusini mashariki mwa Mexico City.

Vifo vimeripotiwa kutokea eneo kubwa la Mexico City na majimbo jirani ya Morelos, Puebla na Mexico.