Serikali ya Ethiopia yamteua afisa wa ngazi ya juu wa TPLF kama Rais wa mpito wa jimbo la Tigray

Getachew Reda, afisa wa ngazi ya juu wa TPLF

Serikali ya Ethiopia leo Alhamisi imesema imemteua afisa wa ngazi ya juu kutoka chama cha waasi wa Tigray, Tigray People’s Liberation Front ( TPLF) kama kiongozi wa mpito wa serikali ya jimbo baada ya makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya kikatili vya miaka miwili.

“Waziri mkuu Abiy Ahmed amemteua Getachew Reda kama Rais wa mpito wa utawala wa jimbo la Tigray,” ofisi ya Abiy imesema katika taarifa kwenye Twitter.

Taarifa hiyo inajiri siku moja baada ya bunge la Ethiopia kukiondoa chama cha TPLF kwenye orodha ya makundi ya kigaidi katika hatua ambayo lilisema itasaidia kuimarisha makubaliano ya amani ya Novemba 2022 kati ya waasi wa TPLF na serikali kuu.

Chama cha TPLF, ambacho kiliwahi kutawala siasa za Ethiopia, kilitajwa rasmi kama kundi la kigaidi mwezi Mei mwaka 2021, miezi sita baada ya vita vya Tigray kuanza.

Getachew, ambaye ni mshauri wa kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael, aliwahi pia kuhudumu kama waziri wa mawasiliano katika serikali kuu chini ya waziri mkuu Hailemariam Desalegn ambaye alitawala kuanzia mwaka 2012 hadi 2018.