Kupitia akaunti yao ya twitter, Jeshi la Polisi la Rwanda walieleza kuwa wanashirikiana na wadau wengine kurejesha utulivu na usalama katika kambi ya wakimbizi ya Kiziba, vyanzo vya habari Rwanda vimeeleza.
“Doria za kawaida zinaendelea kufanyika ndani na nje ya eneo la kambi hiyo kuhakikisha wakimbizi wote wanaishi kwa salama na wakazi wengine wa eneo hilo,” sehemu ya ujumbe huo wa tweet umeeleza.
“Wakimbizi kadhaa waliamua kuleta vurugu, wakitupa mawe na kuwashambulia maafisa wa polisi na vitu venye ncha kali, iliyopelekea kukamatwa kwa watu 23 ambao waliwasilishwa kwa vyombo husika vya usalama kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi. Wakimbizi, kama ilivyo wakazi wote nchini Rwanda, lazima wafuate sheria za Rwanda,” ujumbe huo wa tweet ulieleza zaidi.
Wizara ya Kusimamia Maafa na Wakimbizi mapema April 30 ilitoa tamko juu ya uamuzi wake wa kuivunja kamati ya utendaji ya wakimbizi kama ni hatua mojawapo ya kurudisha usalama na utulivu katika kampi hiyo na maeneo yanayoizunguka.
Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya uchunguzi uliofanywa na wizara hiyo kugundua kuwa kiini cha tatizo hilo katika Kambi ya Kiziba ilikuwa ni kamati hiyo, ambayo ilikuwa imeundwa kusaidia uendeshaji wa kambi hiyo, na badala yake imekuwa ikiwahamsisha wakimbizi kupinga maamuzi ya maafisa wa serikali na taasisi zinazoshirikiana nao, kuwazuilia kuingia katika kambi hizo, na kusababisha vurugu kati ya wakimbizi, na kuifanya kambi hiyo na maeneo yanayolizunguka kuwa hatarishi.