Serikali kuu ya Marekani imefungwa

Rais wa Marekani, Donald Trump

Ijumaa saa sita usiku Rais Trump aliamua kufunga serikali kuu ya Marekani kutokana na madai yake bungeni apatiwe fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico

Baadhi ya idara za serikali kuu ya Marekani zimefungwa mpaka Alhamisi na pengine kuna uwezekano idara hizo zikawa zimefungwa kwa siku kadhaa zaidi au hata wiki kadhaa huku Rais Donald Trump akishikilia msimamo wake akitaka apatiwe fedha kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico na wademocrat wameendelea kupinga vikali suala hilo.

Rais Trump aliandika ujumbe kwenye Twitter siku ya Jumapili “njia pekee ya kusitisha usafirishaji madawa haramu, magenge, usafirishaji magendo ya binadamu, uhalifu na mambo mengine mengi yanayoingia nchini kwetu ni kujenga ukuta”.

Ijumaa saa sita usiku Rais Trump aliamua kufunga serikali kuu kutokana na madai yake kwa ajili ya ujenzi wa ukuta wa mpakani, kiongozi namba mbili wa senate upande wa Democrat Dick Durbin wa Illinois alitweet na kuongezea hii haina maana na ni ukatili. Hii ni mara ya nne katika muda wa miaka mitano kwa bunge la Marekani na White House kushindwa kukubaliana juu ya fedha kiasi gani serikali kuu inaweza kutumia na kwa malengo gani na kusababisha kufungwa kwa baadhi ya shughuli za serikali kuu Marekani.