Serikali ya mpito Libya yaahidi kuitisha uchaguzi Decemba

Viongozi wa ulimwengu kwenye kikao kuhusu Libya kwenye mkutano wa awali Januari 2020, mjini Berlin

Serikali ya mpito ya Libya imesisitiza azma yake ya kuitisha uchaguzi Decemba 24 wakati wa mkutano wa Jumatano  mjini Berlin, huku Ujerumani ambayo ni mwenyeji wa kikao hicho ikisema kuwa itaendelea kutoa shinikizo hadi vikosi vyote vya kigeni viondolewe Libya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Ujerumani pamoja na Umoja wa Mataifa waliyaleta pamoja mataifa 17 kwenye mkutano huo wakati serikali na maafisa wa serikali ya mpito ya Libya wakiandamana na mawaziri wa kigeni wa Misri,Uturuki,Tunisia, Algeria, Ufaransa na Italy.

Miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu waliohudhuria ni waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken pamoja na maafisa kutoka Russia na Umoja wa falme za kiarabu.

Wakati wa kikao hicho, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema kuwa wameingia ukurasa mpya kwa kuwa sasa hawazungumzii kuhusu Libya bali sasa taifa hilo ni miongoni mwa washiriki.

Kikao hicho kimefuatia kile cha 2020, ambapo viongozi walikubaliana kutoyauzia silaha makundi yanayo zozana nchini Libya pamoja na kuyashinikiza kusitisha kabisa mapigano.