Serikali ya Ufaransa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani

Serikali ya Ufaransa inakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani Jumatano, hatua ambayo inaweza kuisumbua serikali ya waziri mkuu Michael Barnier.

Wachambuzi wanatabiri kuna uwezekano mkubwa kwa wabunge wa Ufaransa, kuiunga mkono kura hiyo.

Waziri Mkuu Barnier amewaonya wanasiasa kwamba kuiangusha serikali yake kutaifanya Ufaransa kupitia kipindi kigumu zaidi. Kura hiyo ya kutokuwa na imani ilichochewa na hatua ambayo imechukuliwa kama kwenda kinyume cha katiba, baada ya waziri mkuu Jumatatu, kusogeza mbele bajeti mpaka 2025 bila ya kupitishwa na bunge.

Waziri Mkuu Barnier alijitetea kwamba uamuzi wake huo ulikuwa wa kuleta utulivu wakati huu Ufaransa inapitia mgawanyiko mkubwa wa kisiasa.

Kiongozi huyo ambaye amekuwa madarakani kwa miezi mitatu, anatazamia kuleta udhibiti wa bajeti hiyo yenye nakisi kubwa.