Watawala wa kijeshi wa Niger, Jumapili wamepokea kwa mikono miwili tangazo kwamba Ufaransa, itaondoa vikosi vyake mwishoni mwa mwaka ikiwa ni hatua mpya ya kumiliki dola lao.
Taarifa hiyo imetolewa saa kadhaa baada ya rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kutangaza kwamba Paris, itaomuondoa hivi karibuni balozi wake Niger, na jeshi lake kuondoka baada ya hapo.
Taarifa ya utawala wa kijeshi wa Niger, ilieleza kuwa tumeupokea uamuzi huo ikiwa ni hatua kuelekea kushikilia dola, ikiwa ni muendeleazo wa matukio toka kupinduliwa kwa rais Mohamed Bazoum hapo Julai 26.
Taarifa iliyotolewa na televisheni ya taifa imeendelea kusema kwamba balozi na vikosi vya Ufaransa vitaondoka mwishoni mwa mwaka.
Mapema Jumapili kabla ya tangazo la rais wa Ufaransa, idara ya usalama wa usafiri wa anga barani Afrika (ASECNA) ilitangaza kupigwa marufuku kwa ndege za Ufaransa kuruka juu ya anga ya Niger.