Senegal yatetea utamaduni wake dhidi ya mapenzi ya jinsia moja

Rais wa Senegal Macky Sall

Rais wa Senegal Macky Sall ametetea msimamo wa nchi yake wa kutotambua mapenzi ya jinsia moja alipokutana na Waziri Mkuu wa Canada.

"Bila shaka ninaheshimu msimamo wake wakutetea haki za binadamu, lakini mimi pia ni mtetezi wa haki hizo. Hata hivyo sheria za nchi yetu zinaheshimu misingi ambayo inawakilisha utamaduni na ustarabu wetu."

Hatuwezi kuwambia wananchi wa Senegal ghafla kuwa wahalalishe mapenzi ya watu wa jinsia moja na mambo kama hayo. Kila kitu kina wakati wake na kila watu wanautamaduni wao,” Rais amefafanua.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau anamaliza ziara yake ya Senegal iliyokuwa sehemu ya juhudi zake za kutaka kuungwa mkono na nchi za Afrika ili nchi yake ipate kiti cha muda katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Akiwa huko Senegal Alhamisi kiongozi huyo alitembelea kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ambacho kinatoa mafunzo kwa polisi wanawake katika jeshi, na kuhudhuria maonyesho ya kazi zao.

Kabla ya kuwasili Dakar, Trudeau alitembelea Ethopia na kukutana na viongozi wa nchi za Kiafrika na kuwahimiza kuunga mkono Canada kuweza kupata nafasi yake kwenye baraza la usalama.