Mawakili wanaoliwakilisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) walisema Jumatatu kuwa mfumo wa hifadhi ya Rwanda una mapungufu, kama sehemu ya changamoto kwa sera ya serikali ya Uingereza ya kuwafukuza wanaotafuta hifadhi huko.
Mawakili hao walisema sera hiyo inahatarisha wanaotafuta hifadhi kukabiliwa na mchakato uliopigwa marufuku unaojulikana kama wa kuwarudisha wakimbizi sehemu ambazo wanaweza kuteswa kwa kuzingatia ushahidi wa siku za nyuma ambao ulikuwa sehemu muhimu ya hoja ya Mahakama ya Juu ya Uingereza ilipotoa uamuzi wa mpango wa nchi hiyo kuwa kinyume cha sheria mwaka jana.
"UNHCR inadanganya," msemaji wa serikali ya Rwanda alisema katika taarifa yake siku ya Jumanne.
"Shirika hilo linaonekana kudhamiria kuwasilisha madai ya uwongo kwa mahakama za Uingereza kuhusu Rwanda inavyowahudumia waomba hifadhi, huku likiendelea kushirikiana nasi kuwaleta wahamiaji wa Kiafrika kutoka Libya kwenye usalama nchini Rwanda."