Rwanda yarudi katika masharti magumu ya kudhibithi maambukizi ya Corona

Serikali ya Rwanda imepiga marufuku usafiri wa umma na wa kibinafsi kati ya wilaya na mji mkuu wa Kigali, baada ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Maafisa wa afya hata hivyo wamesema kwamba usafiri wa ndani na nje ya nchi utaendelea lakini wasafiri wanahitajika kuwa na cheti kuonyesha kwamba wamepimwa virusi vya Corona.

Watu 105 walifariki mwezi Desemba mwaka uliopita, na kuwa mwezi ambao ulirekodi idadi kubwa zaidi ya vifo kutokana na virusi vya Corona nchini Rwanda.

Maafisa wana Imani kwamba masharti ya kuzuia usafiri kati ya wilaya yatasaidia kupunguza kiwango cha maambukizi.

Watu 820 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona na 30 kufariki kutokana na virusi hivyo nchini Rwanda

Msimamizi wa afya ya msingi nchini Rwanda Tharcisse Mpunga, ameambia shirika la habari la serikali ya Rwanda kwamba kutokana na kiwango cha maambukizi, Rwanda inastahili kusitisha shughuli za kawaida na watu kulaazimishwa kukaa nyumbani na usafiri wa watu kuingia nchini humo kusitishwa kwa mda wa siku 14 ili kudhibithi maambukizi.

Kulingana na masharti mapya, shughuli zote za biashara zitatakiwa kufungwa saa kumi na mbili jioni saa za Rwanda. Mikutano yote imepigwa marufuku.

Kila mtu anatakiwa kuwa nyumbani kwake ifikapo saa nne usiku hadi saa kumi kamili asubuhi.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC