Rwanda inasema imeboresha haki za binadamu nchini humo

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Serikali ya Rwanda imetangaza kwamba imechukua hatua ya kuboresha haki za binadamu kwa kutekeleza makubaliano ya kimataifa ya Geneva kuhusu haki za binadamu. Nchi hiyo inatangaza hatua hii wakati kukiwepo ukosoaji wa kimataifa kuhusu ukosefu wa uhuru wa kutoa maoni nchini humo.

Akizungumza mjini Kigali waziri wa sheria na mwanasheria mkuu wa Rwanda, Johnston Busingye alisema katika mikataba 50 ya Geneva kuhusu kuheshimu haki za bidamu nchi ya Rwanda imekwishatekeleza mikataba minane kati yake kwa kiwango cha asilimia 100 huku ile iliyosalia ikiendelea kutekelezwa kwa kiwango cha kati ya asilimia 80 hadi 90.

“Tunafurahi kwa sababu tunaendelea kutekeleza kwa kiasi kikubwa makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu kama ilivyosainiwa kule Geneva na tutaendelea kufanya hivyo hadi mikataba yote 50 tuliyosaini tuitekeleze kikamilifu”.

Hata hivyo waziri huyo anatamka haya wakati kukiwepo na madai hasa kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu kuhusu ukosoaji wa haki za binadamu na ukosefu wa uhuru wa kutoa maoni nchini Rwanda jambo ambalo siku zote serikali imekuwa ikipuuza na kulitaja kama uzushi mtupu ambao una nia ya kuipaka serikali matope. Waziri wa sheria alisema wapo watakaoendelea kusemaa lakini jambo la msingi ni kutekeleza majukumu yao.

“Ni wazi watu wataendelea kusema lakini sisi tunasema kwamba tunaendelea kuhakikisha tunatekeleza maazimio hayo yote na tunafurahia pamoja tulipofikia. Ni suala tu la kufanya mambo yetu bila kujali hili wala lile alimradi yote yanakwend sawa".

HRW iliishutumu Rwanda kwa ukiukaji haki za binadamu 2015

Wakati huo huo Andrew Kananga mwanasheria anayetetea haki za binadamu anasema kutokana na hali ilivyo nchini Rwanda hakuna tishio lolote la hatari kwa haki za binadamu kutokana na mabadiliko ya sheria ambayo yamekuwa yakifanywa. “Tukizungumzia mabadiliko ya kisheria kuna sheria nyingi ambazo zimefanyiwa mabadiliko karibu kwenye kila sekta hali inayoashiria uhakika wa kuwepo haki za binadamu na ishara kwamba mazingira yanazidi kuwa bora zaidi”.

Wizara ya sheria ya Rwanda imekuwa ikisema kwamba inajitahidi kuhakikisha kunakuwepo na sheria tetezi kuhusu haki za binadamu lakini hizi bado hazijazima malalamiko ya hapa na pale kuhusu haki za binadamu.