Rwanda imetuma wanajeshi mpakani na DRC na kusema ipo tayari kwa vita

Wanajeshi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo katika mji wa Kibumba, karibu na mpaka na Rwanda, mashariki mwa DRC. Juni 11, 2014

Rwanda imetuma wanajeshi kwenye mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, saa chache baada ya DRC kumfukuza balozi wa Rwanda kwa madai ya DRC kwamba serikali ya rais Paul Kagame inawaunga mkono waasi wa M23.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Alain Mukurarinda amesema kwamba “wakiamua kutangaza vita dhidi ya Rwanda, nasi tupo tayari kuchukua hatua kali, maana hata sasa wanapoendelea kuchukua hatua kama hizo, haina maana kwamba Rwanda imelala usingizi mzito.”

Taarifa ya serikali ya Rwanda ilisema kwamba ‘inasikitishwa na hatua ya DRC kumfukuza balozi Vincent Karega.”

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba “wanajeshi wa Rwanda wameimarisha usalama kwenye mpaka na DRC na wanaendelea kufuatilia hali ilivyo nchini DRC” kufuatia mapigano makali kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa serikali.

Baraza la ulinzi la DRC linaloongozwa na rais Felix Tshisekedi, lilimuamuru balozi wa Rwanda kuondoka nchini humo ndani ya muda wa saa 48, kufuatia ripoti kwamba Rwanda ilikuwa imetuma kikosi maalum cha kijeshi kuwasaidia waasi wa M23 katika sehemu za Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC.

Ripoti za DRC pia zinadai kwamba Rwanda imetuma wanajeshi katika wilaya ya Rubavu, mpakani na DRC kuwasaidia waasi wa M23.

Rwanda imekuwa ikikanusha kila mara, ripoti za kusaidia waasi wa M23 na kusisitiza kwamba kinachoendelea DRC ni swala la usalama wa ndani ambalo lazima lishughulikiwe na serikali ya Kinshasa.

Madai ya serikali ya Rwanda

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa serikali ya Rwanda amesema kwamba “ushirikiano unaendelea kati ya jeshi la DRC na waasi wa FDLR, na jaribio lao la kulenga sehemu za mpakani na Rwanda kwa mashambulizi na kueneza habari za chuki kuhusu Rwanda.”

Rwanda imesema kwamba itaendelea kuieleza jumuiya ya kimataifa kuhusu chuki inazodai zinaenezwa na DRC dhidi ya raia wa Rwanda na raia wa DRC wanaozungumza Kinyarwanda, wanaoishi DRC.

Rais wa DRC Felix Tshisekedi Tshisekedi ameamuru maafisa wa usalama kuhakikisha kwamba raia wa Rwanda wasiingie DRC, huku Rwanda ikitaka raia wake kutokwenda DRC.

“Mimi kama msemaji wa serikali ya Rwanda, nawashauri raia wa Rwanda kufikiria mara mbili kabla ya kuingia DRC,” amesema Alain Mukurarinda, msemaji wa serikali ya Rwanda.

Tshisekedi anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusu uhasama kati ya DRC na Rwanda na mapigano ya M23.

Hivi karibuni, Tshisekedi alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi la DRC na kutuma idadi kubwa ya wanajeshi na silaha katika sehemu za Kivu Kaskazini, kupigana na kundi la waasi la M23.

Mashambulizi ya M23

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walijeruhiwa Jumamosi kutokana na shambulizi la kundi la waasi wa M23 katika sehemu ya Kiwanja, Rutshuru, Kivu Kaskazini.

Waasi wa M23 wamekataa kuondoka mji wa Bunagana licha ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwataka kuondoka sehemu hiyo na kuacha mapigano.