Rwanda ilipuuza madai ya Marekani ya shambulizi huko mashariki mwa DRC

Patrick Muyaya, msemaji wa serikali ya DRC. October 10,2022. (Twitter/Patrick Muyaya)

Msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya pia amelishutumu jeshi la Rwanda na kundi la M23 kwa shambulizi nchini humo

Rwanda leo Jumamosi ilipuuza madai ya Marekani kwamba vikosi vyake vilihusika katika shambulio baya dhidi ya kambi ya wakimbizi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Takriban watu kumi waliuawa katika milipuko siku ya Ijumaa kwenye kambi hiyo iliyoko nje kidogo ya mji wa Goma, vyanzo vya ndani vimesema. Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani imesema katika taarifa yake kuwa inalaani vikali shambulio hilo kutoka Rwanda Defence Forces (RDF) na kundi la M23 lililofanyika katika kambi ya Mugunga.

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Patrick Muyaya pia amelishutumu jeshi la Rwanda na wafuasi wake wa kigaidi wa M23 kwa kuhusika na tukio hilo akilielezea katika taarifa aliyoitoa Ijumaa kwenye mtandao wa X.

Wakati huo huo, msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo ameyataja matamshi hayo ya Marekani kuwa hayana msingi, katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, zamani ukijulikana Twitter.