Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal amesema vituo kadhaa vya nishati viliharibiwa na kwamba Russia inajaribu kuwanyima umeme wananchi wa Ukraine kabla ya mwaka mpya.
Hata hivyo, jeshi la Ukraine limesema limefaulu kudhibiti makombora mengi, na hivyo kuepusha uharibifu mkubwa.
“Kulingana na takwimu za awali, jumla ya makombora 69 yalirushwa. Makombora 58 ya adui yalitunguliwa,” mkuu wa jeshi la Ukraine, Jenerali Valeriy Zaluzhniy amesema.
Awali maafisa walisema zaidi ya makombora 120 yalirushwa, kwa mujibu wa Reuters.
Russia imekuwa ikitumia makombora mara kwa mara kulenga miji ya Ukraine, yakiwemo mashambulizi yaliyoharibu vituo vya miundombinu muhimu, licha ya kukanusha kuwa inawalenga raia.