Russia Jumanne imerusha makombora kwenye bandari ya Bahari nyeusi ya Odesa, maafisa wa Ukraine wamesema, wakati Moscow ikijaribu kukwamisha usafirishaji wa silaha muhimu na njia za usambazaji wa bidhaa nchini Ukraine, katika wiki ya 11 ya vita nchini humo.
Jeshi la Ukraine limesema Russia imerusha makombora saba katika mji wa Odesa, yaliyoanguka kwenye kituo cha biashara na ghala, na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watano.
Meya Gennady Thrukanov ametembeleaa ghala hilo na kusema “halikuwa na uhusiano wowote na miundombinu ya kijeshi au vifaa vya kijeshi.”
Hayo ni wakati Bunge la Marekani lilijadili Jumanne mswada wa dola bilioni 40 kama msaada mpya wa kijeshi na kibinadamu kwa Ukraine, ni zaidi ya dola bilioni 33 alizoomba wiki iliyopita rais Joe Biden.