Russia Jumatano imeishtumu Ukraine kutungua kwa makusudi ndege ya kijeshi ya Russia iliyokuwa inabeba wanajeshi 65 wa Ukraine wafungwa wa vita katika mpango wa kubadilishana wafungwa, na kutaja kitendo hicho kuwa cha kinyama na cha kigaidi. Jumla ya watu 74 walifariki katika tukio hilo.
Wizara ya ulinzi ya Russia imesema wahudumu sita na wanajeshi watatu wa Russia walikuwa ndani ya ndege hiyo ya kijeshi aina ya Ilyushin 76 iliyotunguliwa karibu na mji wa Russia wa Belgorod karibu na mpaka wa Ukraine.
“Uongozi wa Ukraine ulijua vyema kwamba, kulingana na utaratibu uliowekwa, wanajeshi wa Ukraine wangesafirishwa na ndege ya kijeshi hadi uwanja wa ndege wa Belgorod leo katika mpango wa ubadilishanaji,” taarifa ya wizara ya ulinzi imesema.
Wizara ya mambo ya nje ya Russia imetaja kitendo hicho kuwa “cha kinyama.”
Mykhailo Podolyak, mshauri wa Rais wa Ukraine ameiambia Reuters “ Maelezo yatatolewa baadaye. Muda unahitajika kufafanua taarifa zote.”