Russia yaanzisha kura ya maoni kuhalalisha kukalia kimabavu majimbo manne ya Ukraine

Mwanajeshi apiga kura katika kituo cha jimbo la Luhansk linalodhibitiwa na waliojitenga na Ukraine, mashariki mwa Ukraine, Septemba 23, 2022. Picha ya AP

Russia Ijumaa imeanzisha zoezi la watu kupiga kura ya maoni kwa lengo la kuhalalisha hatua yake ya kukalia kimabavu majimbo manne ya Ukraine na kuongeza hatari ya vita vilivyodumu kwa miezi saba sasa.

Upigaji kura utaamua iwapo mikoa hiyo inapaswa kuwa sehemu ya Russia ulianza baada ya Ukraine mapema mwezi huu kudhibiti tena maeneo makubwa ya mikoa ya kaskazini mashariki katika mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Russia.

Vita vya Russia vimeua maelfu ya watu, kuwalazimisha mamilioni wengine kukimbia makazi yao na kudumaza uchumi wa dunia.

Huku Rais wa Russia Vladimir Putin akitangaza pia wiki hii rasimu ya kijeshi ya kuandikisha wanajeshi wa akiba 300,000 watakaopigana nchini Ukraine, Kremlin inaonekana kujaribu kuimarisha tena nguvu zake katika mzozo huo mbaya.