IOC yathibitisha kupigwa marufuku shirikisho la riadha Russia.

Rais wa OIC Thomas Bach akitoa hotuba.

Mkutano mkuu wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki, (IOC) uliofanyika Jumanne mjini Lausanne, umethibitisha kupigwa marufuku kwa shirikisho la riadha la Russia, lakini pia ukaacha nafasi wazi kwa warussia kushiriki katika baadhi ya michezo kwenye mashindano ya Olimpiki ya mwaka huu mjini Rio De Jeneiro, Brazil.

Akizungumza baada ya mkutano huo, rais wa IOC, Thomas Bach alisema viongozi wa riadha wana wasiwasi mkubwa, kwamba wanariadha wanaotoka katika mataifa yasiyotii sheria za shirikisho hilo, kama vile Kenya na Russia, hawana dosari.

Hata hivyo Bach alisema kwamba hakuna mpango wa kupiga marufuku kwa jumla, kamati ya riadha ya Russia.

Bach alisema kuwa kuna shutuma za udanganyifu kwa wanamichezo wa Kenya na kuongeza kuwa taifa hilo linakabiliwa na changamoto sawa na Russia, za kuhakikisha kwamba wanariadha wote wana nafasi sawa wakati wa Olimpiki mjini Rio De Jeneiro.